Uncategorized

Siasa ni za sasa tu!

Muda nao mewadia, wakwenda uchaguzini
Wengi nao taridhia, hadi vijitongojini
Agosti mekaribia, na wema tuchagueni
Siasa ni za sasa tu! Usihadaiwe.

Sikubali kupigia, kelele wako pinzani
Wala kumkaripia, kwa hatari taletani
Maovu yatakutia, yako nafsi gerezani
Siasa ni za sasa tu! Usihadaiwe.

Meanza kukaribia, tangu ianze kampeni
Harambee kuchangia, ndo zako hukosekani
Wajinga wapumbazia, wajanja twaelewani
Siasa ni za sasa tu! Usihadaiwe

Nini ulitufanyia, ulipokuwa kitini?
swali hili tasalia, hadi Agosti mwanzoni
Na ulizoahidia, umetutimiziani?
Siasa ni za sasa tu! Usihadaiwe.

Nduguze sikilizia, kura zichungeni
Bwenyenye kutumikia, mameni makinikeni
Usoni makinikia, Agosti tuamueni
Siasa ni za sasa tu! Usihadaiwe.

Stephen Mburu
Malenga wa michepuko.

2 thoughts on “Siasa ni za sasa tu!”

Leave a comment